Chozi La Damu

Kwaya Ya Mt.Kizito

Watoto wa nyumba zote njooni tuungane
Tuwalilie wazazi chozi la damu
Tupaaze sauti zetu za majonzi na kwikwi
Kwa wachache wenye huruma watatusikia
Haki ya malezi bora tumenyang'anywa
Urithi wa maadili tumefutiwa
Oh dunia dunia, dunia unatutesa
Oh dunia dunia, tumekukosea nini
Oh dunia dunia, mbona hupendi watoto
Oh dunia dunia, sikia kilio chetu
1. Oh dada zetu na mama zetu, tunajua mnajipenda
Ingawaje tungetamani na sisi mtufikirie
Mavazi mnayovaa leo yanatufundisha nini
Mnafikiria nini kwa kizazi mnachokilea
Msije mkashangaa dunia siku zinazokuja
Viwanda vyote vya nguo vitakapofungwa
2. Oh kila siku tunapolala baba zetu hamjarudi
Asubuhi tukiamka, baba zetu mmeondoka
Siku tukibahatika kushtuka usiku wa giza
Tunachokishuhudia ni mama anapigwa makofi
Na vitisho vya talaka matusi na harufu ya pombe
Darasa gani mnatupa watoto wenu
3. Oh tukirudi toka shuleni, madaftari hamkagui
Eti kwa kuwa tumechoka, burudani mwatuwekea
Video mnazowasha picha za vita na mauaji
Au mikanda iliyorekodiwa Sodom na Gomora
Hamkumbuki ya kuwa mnayafuta ya darasani
Urithi gani mnatupa wazazi wetu
4. Oh kwenye chakula cha usiku, siku zote baba hayuko,
Kusali sala za pamoja, kwenye nyumba yetu ni mwiko,
Amechelewa kutoka kwa mama mdogo yule wa siri
Au giza likizidi, hatarudi mpaka asubuhi
Na mama akishajua mbio kwa Anko wa usiseme`
Familia moja baba na mama watano
5. Oh kwa sababu ya mambo haya, ndugu zetu wanaumia
Wapo wanaorandaranda mitaani bila makazi
Wengi wamelazimika kuajiriwa bado wadogo
Hawana tena nafasi ya kusoma wapate elimu
Na wengi wanajiuza miili yao ili waishi
Mbona dunia umetugeuka watoto

Lyrics provided by https://damnlyrics.com/